Madaraja ya Singa za Mkonge ni yapi?

1) Daraja la 3L

Urefu wa singa ni sentimeta 90 (futi 3) na kuendelea. Rangi ya singa ni mchanganyiko wa nyeupe na manjano. Singa ni lazima isafishwe na kulainishwa vizuri, isiwe na magome, mafundo, kusokotana na isichanganywe na lapulapu.

2) Daraja la 3 S

Urefu wa singa ni sentimeta 60 (Futi 2) - 89. Rangi ya singa ni mchanganyiko wa nyeupe na manjano. Singa ni lazima isafishwe na kulainishwa vizuri, isiwe na magome, mafundo, kusokotana na isichanganywe na lapulapu.

3) Daraja la UG (AU R)

Urefu wa singa ni sentimeta 60 (futi 2) na kuendelea. Rangi ya singa ni ya kufifia na kijanikijani iliyosababishwa na uhaba wa maji wakati wa kusindika,kuchelewa kukauka hususan majira ya mvua au kuchelewa kusindikwa . Singa ni lazima isafishwe na kulainishwa barabara, isiwe na magome, mafundo, kusokotana na isichanganywe na lapulapu.

4) Daraja La SSUG

Hii ni singa isiyokidhi sifa za daraja la UG, lakini inayoweza kuuzwa hata katika masoko ya nje ya nchi. Urefu wa singa usiwe chini ya sentimeta 60 (60cm=2ft). Rangi ya singa inaweza kuwa ya kimanjano hadi iliyofifia sana na yenye madoadoa mengi. Lakini singa ni lazima iwe imesafishwa na kulainishwa barabara, isiwe na magome ya aina yoyote ile, mafundo, kusokotana, singa iliyooza na isichanganywe na lapulapu.

5) TOW (LAPULAPU)

Hizi ni singa zilizokatika wakati wa kupiga brashi na kutupwa nyuma ya mashine ya kayamba. Rangi yake iwe ya samli nyeupe. Isiwe na magome, mafundo, mavumbi na isichanganywe na vipande vya singa za madaraja mengine.

 

6) UF (UNSPINNABLE FIBRE OR UNEXPORTABLE FIBRE)

Singa za daraja hili zina urefu usiopungua sentimita 60 na kuendelea na rangi yake huwa ya weusi au kahawia.

Singa za daraja hili kwa kawaida hutawaliwa na maganda, mafundo na takataka nyingi na wakati mwingine hutawaliwa na madoadoa mengi na hata kuoza. Hii ni singa ambayo haiwezi kuwekwa kwenye madaraja yaliyotajwa hapo juu.

7) UHDS

Hii ni singa inayozalishwa kienyeji kutokana na zana duni za uchakataji wa majani ya Mkonge. Mfumo huu wa uchakataji ni maarufu zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Kwa kawaida singa inayozalishwa huwa ni ya daraja la chini zaidi ya madaraja yaliyotajwa hapo juu. Sifa ya singa hii ni kuwa na magome, mafundo, takataka nyingi na mara nyingi rangi yake ni mchanganyiko wa manjano iliyofifia na weusi. Urefu ni sentimeta 60 na kuendelea.

 

Taasisi Shirikishi
Hakimiliki ©2026 Bodi ya Mkonge Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.