MENEJIMENTI YA TSB YAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO WA E-OFFICE

Imewekwa: 09 Oct, 2025
MENEJIMENTI YA TSB YAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO WA E-OFFICE
Menejimenti ya Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Saddy Kambona, imepatiwa mafunzo maalum juu ya matumizi ya mfumo wa e-Office ili kuwawezesha kuanza rasmi kutumia mfumo huo katika shughuli za kila siku za ofisi. Mafunzo hayo  yameendeshwa na Maafisa kutoka Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Ndg. Sigfrid Ngowi kwa kushirikiana na Ndg. Modestus Sikada. Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Ndg. Ngowi alieleza kuwa e-Office ni mojawapo ya mifumo rasmi ya mawasiliano Serikalini, yenye lengo la kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.   Aliongeza kuwa mfumo huo unapunguza utegemezi wa karatasi na kuongeza matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika usimamizi na utunzaji wa nyaraka za kiofisi. Mfumo wa e-Office unatajwa kuwa nyenzo muhimu katika mageuzi ya utendaji kazi wa Serikali ya Kidijitali. Kupitia mfumo huu, taasisi za umma kama Bodi ya Mkonge Tanzania zinatarajiwa kuboresha ufanisi wa kazi, kuongeza uwazi, na kuchangia katika utekelezaji wa ajenda ya Serikali Mtandao, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa taifa la kidijitali lenye utawala bora na huduma bora kwa wananchi.
Taasisi Shirikishi