ELIMU YA MKONGE YACHOCHEA HAMASA MPYA KWA WAKULIMA WA CHALINZE
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) imetoa elimu kwa wakulima wadogo wa Mkonge wa Chalinze kuhusu mbinu bora za kilimo cha Mkonge chenye tija, kinachozingatia kanuni sahihi za kilimo bora na endelevu.
Mafunzo hayo yalitolewa na Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge kutoka TSB, Bw. Simon Kibasa, wakati wa kikao cha mwaka cha wadau wa zao la Mkonge cha Halmashauri ya Chalinze kilichofanyika tarehe 14 Oktoba, 2025 katika kijiji cha Mdaula.
Katika mafunzo hayo, Bw. Kibasa alielekeza wakulima njia bora za upandaji wa Mkonge, namna ya kukabiliana na magonjwa yanayoweza kushambulia zao hilo, pamoja na mbinu za kuongeza thamani na masoko.
Amebainisha kuwa kufuata kanuni sahihi za kilimo cha Mkonge kutawawezesha wakulima kuongeza uzalishaji, kwani kiwango cha uzalishaji wa Mkonge duniani bado kiko chini licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa zao hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa WAMKOCHA AMCOS, Bw. Burton Nsape, aliishukuru Bodi ya Mkonge Tanzania kwa kufika na kutoa elimu hiyo muhimu, akisema kuwa wakazi wa Chalinze wamehamasika zaidi kuingia katika kilimo cha Mkonge na kuomba wataalamu wa Bodi kuendelea kuwatembelea mara kwa mara ili kukuza uelewa na ufanisi katika kilimo cha Mkonge.
Kupitia mafunzo hayo, wakulima wamepata uelewa wa mbinu bora za upandaji, uchakataji na uuzaji wa Mkonge, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza uzalishaji, kipato na tija katika sekta ya Mkonge nchini.








