TSB YATOA MAFUNZO YA KILIMO BORA CHA MKONGE HAYA MODERN AGRICULTURE

Imewekwa: 18 Sep, 2025
TSB YATOA MAFUNZO YA KILIMO BORA CHA MKONGE HAYA MODERN AGRICULTURE

Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) imetoa mafunzo ya kilimo bora cha Mkonge kwa watendaji na wafanyakazi wa Shamba la Haya Modern Agriculture lililoko Korogwe, mkoani Tanga. Mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati ya TSB kuhakikisha Sekta ya Mkonge inazalisha kwa tija na kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo.

Akiongoza mafunzo hayo, Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge, Bw. Simon Kibasa, alielekeza namna ya kuandaa shamba, kuchagua mbegu bora, njia za upandaji, magonjwa yanayoweza kushambulia Mkonge sanjari na mpango wa uvunaji Mkonge.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo Msimamizi wa Shamba la Haya Modern Agriculture, Bw. Yusufu Bilali, amesema elimu waliyoipata imekuwa chachu ya kuboresha mwenendo wa kilimo shambani, hasa katika eneo la uandaaji na matumizi sahihi ya mbegu.

“Awali tulikuwa tunachukulia matumizi ya mbegu ni mbegu tu, bila kujali ubora wake. Lakini kutokana na elimu tuliyoipata leo siku nyingine tukilima na kupanda tutapanda kwa usahihi zaidi.,” amesema Bw. Bilali.

TSB inaendelea kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Mkonge nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza zao hili la kimkakati
Taasisi Shirikishi