TSB YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA KUPITIA SEMINA YA MAADILI KWA WATUMISHI
Watumishi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) wamepatiwa semina ya maadili ya utumishi wa umma na mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uwajibikaji, uadilifu na utendaji kazi wenye kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Semina hiyo ilifanyika tarehe 21 Mei 2026, katika ofisi za Bodi ya Mkonge jijini Tanga na kuendeshwa na Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, Bw. Frank Mapunda.
Akitoa mada katika semina hiyo, Bw. Mapunda amesema kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mtumishi wa umma na kwamba uadilifu pamoja na kuzingatia maadili ya kazi ni msingi muhimu katika kujenga taasisi yenye uwazi, uwajibikaji na huduma bora kwa wananchi.
Aidha, amewasisitiza watumishi wa TSB kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma ili kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi hii.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Bw. Olivo Mtung’e, ameishukuru TAKUKURU kwa kutoa elimu hiyo muhimu kwa watumishi wa Bodi ya Mkonge na kueleza kuwa semina hiyo imekuja kwa wakati muafaka katika kuendelea kujenga utamaduni wa uwajibikaji na utendaji wenye kuzingatia maadili ndani ya taasisi.








