BALOZI SULEIMAN AWAITA WADAU WA MKONGE CHINA
Balozi wa Tanzania nchini China, Dkt. Suleiman Haji Suleiman, amewataka wakulima na wafanyabiashara wa Mkonge nchini kuongeza juhudi kuzalisha Mkonge kwa wingi bila kuhofia masoko kimataifa hususani nchini China huku akiwataka kutembelea nchini humo ili kujionea fursa mbalimbali.
Akizungumza wakati alipotembelea Banda la Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ambapo ameipongeza TSB kwa jitihada zake zinazofanikisha ongezeko la uzalishaji mwaka hadi mwaka.
"Soko la Mkonge nchini China ni kubwa na linaendelea kuhitaji malighafi hiyo, hivyo nawasihi Watanzania kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji bila kuhofia mauzo. Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini China iko tayari kuwasaidia wazalishaji na wafanyabiashara wa Mkonge kutafuta masoko na kuwaunganisha na wanunuzi nchini China," amesema Balozi Dkt. Suleiman.
Pamoja na mambo mengine, amesisitiza kuwa kila Mtanzania mwenye nia ya kuwekeza au kuuza Mkonge katika Soko la China atapata ushirikiano kutoka ofisi ya ubalozi ili kuhakikisha ananufaika na fursa hizo.








