FURSA KUBWA ZA UWEKEZAJI ZIPO: SOKO LA DUNIA LAHITAJI TANI 500,000 HADI 600,000 ZA MKONGE KWA MWAKA

Imewekwa: 11 Jul, 2026
FURSA KUBWA ZA UWEKEZAJI ZIPO: SOKO LA DUNIA LAHITAJI TANI 500,000 HADI 600,000 ZA MKONGE KWA MWAKA

Zao la mkonge linaendelea kujidhihirisha kuwa miongoni mwa mazao yenye fursa kubwa za kiuchumi nchini Tanzania, huku mahitaji ya soko la dunia yakizidi kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa sasa wa nchi. Hali hiyo inaashiria uwepo wa nafasi kubwa kwa wawekezaji na wakulima kuongeza uzalishaji na thamani ya zao hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Masoko wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Bw. Best Rukanda, alisema Tanzania kwa sasa huzalisha takribani tani 72,000 za mkonge kwa mwaka, wakati mahitaji ya soko la dunia yanafikia kati ya tani 500,000 hadi 600,000 kwa mwaka.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na mazingira yanayofaa kwa kilimo cha mkonge, hususan katika mikoa ya Tanga na Morogoro, jambo linaloifanya nchi kuwa na uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji na kukidhi sehemu ya mahitaji makubwa ya soko la kimataifa.

Bw. Rukanda alieleza kuwa mkonge ni zao la kimkakati linalotumika kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye thamani kubwa, ikiwemo kamba, mikoba, viatu, mazulia, karatasi maalumu na hata noti. Kutokana na matumizi hayo, zao hilo lina mchango mkubwa katika kukuza viwanda, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa Taifa.

Aidha, alisema China ndiyo soko kuu la mkonge wa Tanzania, huku katika bara la Afrika masoko makubwa yakipatikana nchini Nigeria, Ghana, Morocco, Misri na nchi nyingine za Afrika Magharibi.

Bw. Rukanda aliwahimiza Watanzania na wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani wa zao la mkonge ili kuongeza tija, kuchochea ukuaji wa viwanda, kuzalisha ajira na kuongeza mapato ya Taifa kupitia mauzo ya nje na upatikanaji wa fedha za kigeni.

Taasisi Shirikishi
Hakimiliki ©2026 Bodi ya Mkonge Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.