SHERIA YA TASNIA YA MKONGE YAFANYIWA MAREKEBISHO

Imewekwa: 28 Aug, 2026
SHERIA YA  TASNIA YA MKONGE YAFANYIWA MAREKEBISHO

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Godfrey Chongolo (Mb), amewasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kilimo wa Mwaka 2026 (The Agricultural Laws Amendments Act, 2026) katika Kikao cha Pili cha Mkutano wa Nne wa Bunge la 13, kilichofanyika tarehe 27 Agosti 2026, jijini Dodoma.

Muswada huo unapendekeza marekebisho ya sheria mbalimbali zinazosimamia sekta ya kilimo, ikiwemo Sheria ya Tasnia ya Mkonge, Sura ya 30; Sheria ya Usalama wa Chakula, Sura ya 249; Sheria ya Tasnia ya Sukari, Sura ya 251; na Sheria ya Tasnia ya Chai, Sura ya 275.

Akielezea madhumuni ya marekebisho hayo, Mhe. Chongolo amesema yanakusudia kuondoa mapungufu yaliyobainika katika utekelezaji wa baadhi ya masharti ya sheria hizo, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi na utekelezaji wa sheria hizo.

Marekebisho ya Sheria ya Tasnia ya Mkonge

Miongoni mwa sheria zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Tasnia ya Mkonge, Sura ya 30, ambapo Serikali imependekeza mabadiliko yatakayolenga kuimarisha usimamizi wa shughuli mbalimbali katika Tasnia ya Mkonge.

Kwa mujibu wa Muswada huo, inapendekezwa kuhamisha mamlaka ya kutunga kanuni zinazohusu uchakataji, usafirishaji nje ya nchi na uhifadhi wa mkonge kutoka kwa Bodi ya Mkonge Tanzania kwenda kwa Waziri mwenye dhamana ya Kilimo. Mapendekezo hayo yameainishwa katika Sehemu ya Tatu ya Muswada, na yanahusisha marekebisho ya Vifungu vya 5 na 22 vya Sheria ya Tasnia ya Mkonge, Sura ya 30.

Mhe.Chongolo amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha utekelezaji wa masharti ya Sheria kwa ufanisi zaidi, pamoja na kuboresha mfumo wa usimamizi wa shughuli zinazohusiana na Tasnia ya Mkonge. Aidha, Muswada unapendekeza kurekebishwa kwa Kifungu cha 2 cha Sheria kwa kuongeza fasili ya msamiati “shared function”, kwa lengo la kutoa ufafanuzi zaidi wa maana ya neno hilo linapotumika katika Sheria.

Vilevile, inapendekezwa kuongezwa kwa Kifungu kipya cha 24A, kitakachoweka masharti kuhusu ufifilishaji wa makosa yaliyoainishwa chini ya Sheria ya Tasnia ya Mkonge. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mhe. Chongolo, kifungu hicho kinakusudia kurahisisha na kuharakisha mchakato wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makosa mbalimbali yanayoweza kujitokeza katika Tasnia ya Mkonge.

Kwa ujumla, marekebisho yanayopendekezwa katika Sheria ya Tasnia ya Mkonge yanatarajiwa kuimarisha mfumo wa kisheria na usimamizi wa tasnia, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sheria na kuweka mazingira wezeshi kwa wadau kushiriki kikamilifu katika maendeleo endelevu ya zao la mkonge nchini.

Taasisi Shirikishi
Hakimiliki ©2026 Bodi ya Mkonge Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.